NHK WORLD > Jifunze Kijapani > Mwanzo wa ukurasa wa Kiswahili > Mwalimu Tufundishe > Namna ya kuonyesha mifano kwa kutumia TARI (Somo la 37)

Mwalimu Tufundishe

Namna ya kuonyesha mifano kwa kutumia TARI (Somo la 37)

Unapotoa mifano miwili ama mitatu miongoni mwa vitendo kadhaa, unatumia vitenzi vya umbo la TA na kuongeza RI baada ya kila kitenzi cha umbo la TA kwa mfuatano. Mwishoni, unamalizia sentensi kwa kutumia SHIMASU (nafanya), SHIMASHITA (nilifanya), au SHITAI DESU (ninataka kufanya).

Kwa mfano kwenye mazungumzo ya somo la leo, Anna alifanya mambo mengi alipokuwa Shizuoka. Miongoni mwayo, alimuelezea mama msimamizi wa bweni kwa kutoa mifano miwili, kuwa aliona mlima Fuji na akala sushi.

Anapozungumzia Mlima Fuji, anatumia umbo la TA la kitenzi MIMASU (kuona), ambalo ni MITA, kisha anaongeza RI kwenye neno hilo, na kusema MITARI. Anapozungumzia sushi, anatumia umbo la TA la TABEMASU (kula), ambalo ni TABETA, akaongeza RI kwenye neno hilo na kusema TABETARI.

Kwa pamoja , “Niliona Mlima Fuji, nikala sushi na kadhalika ” inakuwa FUJI-SAN O MITARI, OSUSHI O TABETARI SHIMASHITA.

Anna alipokuwa ziarani alifanya haya na mengineyo. Ikiwa utatumia TARI kuorodhesha kile unachofanya au ulichofanya, unaweza kuonyesha kwamba, ulifanya pia mambo mengine.
Vilevile TARI ina matumizi mengine. Ikiwa utaorodhesha vitendo vyenye maana kinyume kwa wakati mmoja kwa kutumia TARI, unamaanisha ya kwamba unafanya vitendo hivyo mara kwa mara. Kwa mfano, “ninakwenda na kurudi mara kwa mara” ni ITTARI KITARI SHIMASU. Na ukitaka kusema “nawasha na kuzima taa mara kwa mara” ni TSUKETARI KESHITARI SHIMASU.
*Utatoka kwenye tovuti ya NHK.