NHK WORLD > Jifunze Kijapani > Mwanzo wa ukurasa wa Kiswahili > Mwalimu Tufundishe > Umbo la uwezekano la vitenzi (Somo la 35)

Mwalimu Tufundishe

Umbo la uwezekano la vitenzi (Somo la 35)

Umbo la uwezekano la vitenzi huwa na maana mbili.

Moja ni uwezo wa kufanya kitu. Kwa mfano, ikiwa unataka kusema, “Ninaweza kuongea Kijapani,” unatumia umbo la uwezekano la HANASHIMASU (kuongea), ambalo ni HANASEMASU (naweza kuongea).

Maana nyingine ni ruhusa ya kufanya kitu katika mazingira fulani. Kwa mfano, ikiwa unataka kusema “unaweza kutumia kadi ya kufanyia manunuzi,” unatumia umbo la uwezekano la TSUKAIMASU (kutumia), ambalo ni TSUKAEMASU (unaweza kutumia).

Lakini siyo vitenzi vyote vinaweza kunyambulika katika umbo la uwezekano. Vile ambavyo havihusishi dhamira ya mtu haviwezi kubadilika katika umbo hili kama vile FURIMASU yaani kunyesha.

Sasa, acha nikufahamishe namna ya kutengeneza umbo la uwezekano. Kwanza, vitenzi ambavyo silabi kabla tu ya MASU ina irabu E. Hapa, kabla ya MASU, unaweka neno RARE. Kwa hiyo, TABEMASU (kula), inabadilika na kuwa TABERAREMASU (naweza kula).

Pili ni kuhusu vitenzi ambavyo silabi kabla tu ya MASU ina irabu I. Kuna namna mbili. Namna ya kwanza ni kubadilisha I na kuwa E. Kwa hiyo, HANASHIMASU (kuongea), inabadilika na kuwa HANASEMASU (naweza kuongea). TSUKAIMASU (kutumia), inabadilika na kuwa TSUKAEMASU (naweza kutumia). Kwa namna nyingine, unaweka RARE kabla ya MASU. MIMASU (kuona), inabadilika na kuwa MIRAREMASU (naweza kuona).
Baadhi ya vitenzi havifuati namna hizi. KIMASU (kuja), inabadilika na kuwa KORAREMASU (naweza kuja). SHIMASU (kufanya), inabadilika na kuwa DEKIMASU, (naweza kufanya). Kwa hiyo kumbuka maneno hayo.
Tafadhali tembelea ukurasa wa "nyezo za kujifunzia."
*Utatoka kwenye tovuti ya NHK.