NHK WORLD > Jifunze Kijapani > Mwanzo wa ukurasa wa Kiswahili > Mwalimu Tufundishe > Vionyeshi (Somo la 3)

Mwalimu Tufundishe

Vionyeshi (Somo la 3)

Vionyeshi ni maneno tunayoyatumia iwapo tunaonyesha vitu, watu au mahali. Vinaitwa maneno ya KO-SO-A-DO, ambayo yanachukua silabi ya kwanza ya vionyeshi vya makundi manne. KORE (hii), KOKO (hapa), na KONO (hii, linalokuja kabla ya nomino kwa Kijapani), maneno hayo yanaanza na KO, na yako katika kundi la KO. Yanaonyesha vitu, watu au mahali ambapo ni karibu na mzungumzaji.

SORE (hiyo), SOKO (hapo) na SONO (hiyo, linalokuja kabla ya nomino kwa Kijapani), maneno hayo yapo katika kundi la SO. Kundi hili linaonyesha vitu, watu au mahali karibu na msikilizaji. Lakini ikiwa mzungumzaji na msikilizaji wako karibu na kila mmoja, vionyeshi hivyo huashiria vitu, watu au mahali ambapo wako mbali napo kidogo.
ARE (ile), ASOKO (pale) na ANO (ile, linalokuja kabla ya nomino kwa Kijapani), maneno hayo yapo katika kundi la A. Yanaashiria vitu, watu au mahali ambapo ni mbali kutoka mzungumzaji na msikilizaji.

Na DORE (ipi), DOKO (wapi) na DONO (ipi, linalokuja kabla ya nomino kwa Kijapani), maneno hayo yako katika kundi la DO.

Unapoashiria uelekeo, unasema KOCHIRA (upande huu), SOCHIRA (upande huo), ACHIRA (upande ule), na DOCHIRA “upande upi.”

Maneno ya KO-SO-A-DO ni muhimu na mara nyingi huwa yanatumika.
*Utatoka kwenye tovuti ya NHK.