NHK WORLD > Jifunze Kijapani > Mwanzo wa ukurasa wa Kiswahili > Mwalimu Tufundishe > Umbo la kuonyesha nia la vitenzi (Somo la 26)

Mwalimu Tufundishe

Umbo la kuonyesha nia la vitenzi (Somo la 26)

GANBARÔ, (Tujitahidi), ni aina ya mnyambuliko wa vitenzi unaofahamika kama “umbo la kuonyesha nia.” Inaelezea dhamira ya mzungumzaji. Pia hutumika kumshirikisha msikilizaji kufanya jambo fulani pamoja au kumtaka afanye jambo fulani. Huwezi kutumia usemi huu kwa wakuu wako.
Sasa hebu nikueleze namna ya kutengeneza umbo la kuonyesha nia kutoka umbo la MASU. Kwanza, ikiwa irabu ya silabi kabla tu ya MASU inamalizikia na " E," unabadilisha MASU na kuwa YÔ. Kwa mfano, TABEMASU (Kula) inabadilika na kuwa TABEYÔ, (Tule/ Nitakula).

Pili, ikiwa irabu kwenye silabi kabla tu ya MASU inamalizikia na "I," kuna namna mbili ya kunyambua.

Namna ya kwanza, unabadilisha MASU na kuwa YÔ. OKIMASU (kuamka) inageuka na kuwa OKIYÔ (Tuamke). SHIMASU (kufanya) inabadilika na kuwa SHIYÔ (Tufanye au Nitafanya).

Namna ya pili, unaondoa MASU, badilisha irabu "I" kwenye silabi kabla tu ya MASU na kuwa "O," na uongeze U. Mfano ni GANBARIMASU (Nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu). Inabadilika na kuwa GANBARÔ (Tujitahidi kadiri ya uwezo wetu; Nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu). Kuwa makini. Matamshi ni GANBARÔ, hata kama linaandikwa GA-N-BA-RO-U.

Kuna neno moja ambalo linakiuka mtiririko niliokufahamisha. KIMASU (kuja) inabadilika na kuwa KOYÔ.
Angalia "Nyenzo za kujifunzia."
*Utatoka kwenye tovuti ya NHK.